
Yawezekana kuwa si jambo lililotarajiwa kutokea ktk siku za karibuni,lakini ukweli ni kwamba kundi la 'Wateule' linarejea upyaaaa....na tayari memba waliokuwa wakiunda kundi hilo tayari wamemesharekodi nyimbo nne. Unaweza usiamini kinachotokea lakini Jahffarai ambaye alikuwa akiongea kwa niaba ya wenzake anasema.... "Pini ambazo tumesharekodi hadi hivi sasa ni 'Tumetoka Mbali`, `Msela`, `Bado Yuko Vilevile` na `Mtaani Kuna Njaa`.....na albam inakuja,`` . Rapa huyo alisema ufufuko huo wa Wateule unahusisha muungano mpya wa memba wa kundi hilo - Jaymoe, Mchizi Mox, Kevin Kimali, yeye mwenyewe Jaffarai na Solo Thang ambaye kwa sasa anaishi Uingereza. .....``Katika pini hizi za kwanza tumerekodi sisi wanne bila ya kumshirikisha Solo Thang, lakini mipango inafanywa ili kumtumia beats ili atie mistari yake katika nyimbo zinazofuata. ``Marejeo haya ni `sirias` na tunatarajia kuwashirikisha wakali wa Afrika Mashariki kwa kuwa lengo letu sasa ni kusonga mbele.`` ``Ninapokwambia kuwa marejeo haya ni `sirias` ni kwamba ninamaanisha hivyo, wakati wowote tutaanza kurekodi video yetu ya kwanza ya wimbo wa `Mtaani Kuna Njaa` na muda mfupi baadaye tutaachia pini la kwanza la utambulisho katika vituo vya radio,`` alisema Jaffarai. ``Tumeungana kufanya kazi pamoja kwa mara nyingine kwakuwa tunafahamu nguvu kubwa iliyokuwepo ya kundi letu kabla ya kumeguka. Nadhani unaweza kuwa na japo picha ya nini kitatokea vinapokaa vichwa hivi pamoja,`` alisema. Kuungana upya kwa memba wa Wateule kunaashiria jambo. MWAKA WA MALAIKA? Pengine `mwaka wa shetani` ulioimbwa na rapa wa TMK Wanaume Family Mheshimiwa Temba baada ya kushuhudia makundi kibao yakivunjika umefikia tamati. Pengine TMK Wanaume Family na Wanaume Halisi nao wataungana upya mwaka huu, au MwanaFA na AY watarejea kwa kamanda wao wa zamani King Crazy GK wa EastCoast Team. Au Ferooz na Daz Baba wataungana tena kuliteremsha upya majini jahazi lao la Daz Nundaz. Nani ajuaye ya kesho? Lakini kuungana upya kwa Wateule, bila ya shaka, ni jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa hip hop kwasababu wanajua. Wanajua nini wanachotarajia kutoka kwa wakali hao wa mistari waliotambulishwa katika gemu mwaka 2000 kupitia wimbo wao wa ?Hip Hop na Ragga?. WATU KIBAO Wimbo wa `Hip Hop na Ragga` ulikuwa ni kazi ya kwanza na ya mwisho kubwa kwa kundi hilo ambalo liliundwa baada ya wakali hao kukutana kwa mtayarishaji wa muziki P-Funk kwa lengo la kurekodi nyimbo - kila mtu wa kwake - kufuatia ofa waliyopata baada ya kushinda mashindano ya vipaji vya muziki ya Pilsner Ice Pop Stars 2000. Kundi la Sower Cellibas lililoundwa na Jaymoe, Mchizi Mox na Kevin Kimali lilikuwa limeshinda katika kategori ya hip hop, na Solo Thang aliibuka wa pili baada ya kuyapiku makundi na wasanii mbalimbali kama HBC, BDP na Inspektah Haroun. Mark II B alikuwa wa kwanza katika kategori ya Ragga akifuatiwa na Lady Lou, katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mambo Club. ``Ushindi wa kila msanii ama kundi ulitupatia nafasi ya kurekodi wimbo katika studio ya Bongo Records,`` anakumbuka Jaffarai. ``Lakini tukiwa pale studio kwa ajili ya kurekodi wimbo kwa kila mshindi, prodyuza P-Funk alionekana kama kuingia hofu kama tutaweza kufanya vizuri kama kila mmoja atarekodi kivyake, akatushauri turekodi pamoja. ``Kwa sababu ulikuwa ni muunganiko wa wasanii wa hip hop na wa ragga, tukaamua kuuita wimbo huo ?Hip Hop na Ragga`. ``Baada ya kurekodi na prodyuza kukubali kuwa `pini` limetulia, alitushauri tutafute jina na tuendelee kufanya kazi pamoja. ``Wakati tukijiuliza tutumie jina gani, ndipo Kevin Kimali alipotoka na jina hili la Wateule akimaanisha washindi baada ya shindano la pop stars. ``Kundi likaundwa na wasanii saba Mchizi Mox, Kimali, Solo Thang, Jaymoe, Lady Lou, Mark II B na mimi (Jaffarai).`` Muda mfupi baadaye, Solo Thang akajitoa ili afanye kazi kivyake, akifuatiwa na Jaymoe, Lady Lou na Mark II B na kuwaacha wasanii watatu - Mox, Jaffarai na Kimali - ambao wakarekodi katika studio ya MJ Records nyimbo za `Nipende Nichukie`, na ?Watu Kibao? iliyowatoa kiukweli. Katika marejeo, Wateule hawajasahau njia walizopitia awali. Ndiyo maana wamerekodi kwa MJ na pia kwa P-Funk. ``Na tuna nyimbo tutazirekodi nchini Kenya na Uganda,`` alisema Jaffarai. Hata hivyo Jahffarai anasema kurejea kwao hakutawashirikisha wenzao wawili Lady Lou na Mark II B...ambao wao wameamua kukaa mbali na muziki kwa miaka mingi sasa.
No comments:
Post a Comment